Saturday, 2 April 2016

Trump ‘ajipendekeza’ kwa wakuu Republican

Mgombea urais anayeongoza katika chama cha Republican nchini Marekani Donald Trump amechukua hatua ya kushangaza akijaribu kuimarisha uhusiano uliodorora kati yake na wakuu wa chama hicho.

Mfanyabiashara huyo tajiri kutoka New York ametembelea Kamati Kuu ya Taifa ya Republican.
    Trump ayumbayumba kuhusu utoaji mimba

Amechukua hatua hiyo siku moja baada ya kuwakera viongozi hao kwa kusema kwamba hatatii makubaliano ya kuunga mkono mgombea mwengine, iwapo yeye mwenyewe hatashinda uteuzi wa chama hicho.

Bw Trump, anayeongoza kwa wajumbe kwa sasa, amekosoa kile anachosema ni juhudi zisizo za kidemokrasia za kutaka kumpkonya ushindi katika mkutano mkuu wa kuidhinisha mgombea mjini Cleveland mwezi Julai.

Paul Makonda aahidi neema kwa waendesha bodaboda

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amekutana na waendesha pikipiki za kubeba abiria maarufu kama Bodaboda mkoani Dar na kuwapa ahadi nono za kuwainua kimaisha kupitia biashara hiyo.

Pamoja na mambo mengine, Makonda ameahidi kuwapa pikipiki bodaboda hao kwa marejesho ya shilingi 25,000 kwa wiki (sawa na shilingi 3,500) kwa siku na baadae kuwaachia wazimiliki wao.

Katika hatua nyingine, Makonda ameahidi kuwatengenezea mpango mzuri  utakaowawezesha bodaboda hao kuingia katikati ya Jiji, tofauti na ilivyo sasa.

Mwakilishi wa Bodaboda, Daud Laurian alitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni zuio la kuingia mjini (CBD) la Machi 3,2014.
“Tumekutana na changamoto nyingi, kwa mfano kutozwa faini kuanzia Sh50,000 hadi zaidi ya 400,000, kukamatwa kinyama na kufukuzwa na magari,” alisema.

Ahadi ya Makonda kuwaruhusu Bodaboda kuingia Jijini ni ukamilifu wa ahadi ya Rais John Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana.

Juzi, Meya mpya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita (Chadema) pia aliahidi kuhakikisha Bodaboda wanaweza kuingia mjini kwa utaratibu maalum.

Polisi Jijini Mwanza Waamuru Kaburi la Marehemu Lifukuliwe

Polisi mkoani Mwanza, ndugu, jamaa na marafiki, juzi, walilazimika kufukua kaburi na kutoa mwili wa Gelinde Masumbuko baada ya kuzikwa na ndugu wa marehemu Said Mussa na kukaa kaburini kwa siku mbili.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya wahudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Mwanza wa Sekou-Toure, kuukabidhi mwili wa Masumbuko kwa ndugu wa Mussa.

Baada ya kukabidhiwa mwili huo, ndugu wa Mussa waliendelea na taratibu na kuuzika katika makaburi ya Nyashana wilayani Ilemela, kabla ya ndugu wa Masumbuko kubaini kuwa mwili wa ndugu yao uliokuwa umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti hauonekani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Justus Kamugisha alisema walilazimika kuingilia kati suala hilo baada ya ndugu wa Masumbuko kuripoti tukio la mwili wa ndugu yao kupotea katika mazingira ya kutatanisha.

“Baada ya uchunguzi kwa kushirikiana na uongozi wa hospitali tulibaini yalifanyaka makosa kwa mwili huo kukabidhiwa kwa ndugu wa marehemu Mussa ambao tayari walishauzika,” alisema.

Uchunguzi huo ulibaini mwili wa Mussa ulikuwa bado umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali hiyo.
“Ilibidi taratibu za kisheria zichukuliwe na mwili wa marehemu Masumbuko kufukuliwa na kukabidhiwa kwa ndugu zake, huku ndugu wa Mussa nao wakichukua mwili wa ndugu yao kwa mazishi mapya,” alisema Kamugisha.

Mkanganyiko huo ulitokea baada ya ndugu wa Masumbuko kutoka Sengerema kufuata mwili katika hospitali hiyo na kuukosa, hali iliyowalazimu kufuatilia ili kujua alikozikwa na taratibu za kuufukua zifuatwe.

Ndugu wa Masumbuko, Finias Elias, alisema walitarajiwa kumzika jana nyumbani kwao wilayani Sengerema.
Ndugu wa marehemu Mussa, Said Mussa alisema waliotumwa kuuchukua mwili wa marehemu walishindwa kumtambua kutokana na kuvimba uso.