Polisi mkoani Mwanza, ndugu,
jamaa na marafiki, juzi, walilazimika kufukua kaburi na kutoa mwili wa
Gelinde Masumbuko baada ya kuzikwa na ndugu wa marehemu Said Mussa na
kukaa kaburini kwa siku mbili.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya wahudumu
wa chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Mwanza wa
Sekou-Toure, kuukabidhi mwili wa Masumbuko kwa ndugu wa Mussa.
Baada ya kukabidhiwa mwili huo, ndugu wa
Mussa waliendelea na taratibu na kuuzika katika makaburi ya Nyashana
wilayani Ilemela, kabla ya ndugu wa Masumbuko kubaini kuwa mwili wa
ndugu yao uliokuwa umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti
hauonekani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Justus
Kamugisha alisema walilazimika kuingilia kati suala hilo baada ya ndugu
wa Masumbuko kuripoti tukio la mwili wa ndugu yao kupotea katika
mazingira ya kutatanisha.
“Baada ya uchunguzi kwa kushirikiana na
uongozi wa hospitali tulibaini yalifanyaka makosa kwa mwili huo
kukabidhiwa kwa ndugu wa marehemu Mussa ambao tayari walishauzika,”
alisema.
Uchunguzi huo ulibaini mwili wa Mussa ulikuwa bado umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali hiyo.
“Ilibidi taratibu za kisheria
zichukuliwe na mwili wa marehemu Masumbuko kufukuliwa na kukabidhiwa kwa
ndugu zake, huku ndugu wa Mussa nao wakichukua mwili wa ndugu yao kwa
mazishi mapya,” alisema Kamugisha.
Mkanganyiko huo ulitokea baada ya ndugu
wa Masumbuko kutoka Sengerema kufuata mwili katika hospitali hiyo na
kuukosa, hali iliyowalazimu kufuatilia ili kujua alikozikwa na taratibu
za kuufukua zifuatwe.
Ndugu wa Masumbuko, Finias Elias, alisema walitarajiwa kumzika jana nyumbani kwao wilayani Sengerema.
Ndugu wa marehemu Mussa, Said Mussa
alisema waliotumwa kuuchukua mwili wa marehemu walishindwa kumtambua
kutokana na kuvimba uso.